Kwanini wasichana hukimbia vyuo vya Ufundi?


Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha katika Mazoezi ya Vitendo
 KWA muda mrefu sasa, baadhi ya wadau wa elimu nchini na wanasiasa, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikosoa elimu inayotolewa nchini  kwamba imekuwa haiwawezeshi wahitimu kushindana katika soko la ajira.Pia,  kutokana na uhaba wa ajira nchini, serikali na baadhi ya wadau wamekuwa wakihimiza suala la vijana kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa kwenye ofisi mbalimbali.

Licha ya ukweli kuwa, pamoja na sekta nyingine zote, ile ya ufundi ndiyo inayotoa zaidi fursa ya watu kujiajiri wenyewe, takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya wanafunzi wanaochagua kujiunga na vyuo hivyo, hasa wasichana ni ndogo mno.

Mwaka 2010, kwa mfano  wanafunzi waliojiunga na vyuo vya ufundi  vya serikali walikuwa  897 ambapo kati yao,  wasichana walikuwa  16, idadi ambayo ni sawa na asilimia 1.78.

Akitangaza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa wakati huo, Profesa Jumanne Maghembe alisema ,“Idadi hii ni ndogo, lakini hao ndio waliochagua fani hiyo au kuwa na sifa za kutosha kuchukua masomo ya ufundi.”

Pia,  mwaka 2011 wanafunzi 916, wasichana wakiwa 55 na wavulana 861 walichaguliwa  kujiunga na mafunzo ya vyeti katika vyuo vya ufundi vya Mbeya (MIST), Dar es Salaam (DIT), Arusha (ATC) na Chuo Maji  Lwegarulira  kilichoko Dar es Salaam.

Lakini,  Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha,  Dk Richard Masika, anakiri kwamba upungufu wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya ufundi ni mkubwa sana hasa kwa upande wa wanafunzi wa kike.
Kwa mujibu wa  Dk Masika, mwaka jana zaidi ya wanafunzi 100 walihitimu kozi mbalimbali za ufundi chuoni hapo na kuwa, kati yao kulikuwa na wasichana wanane pekee.

“Ukijaribu kuangali kwa makini, utagundua kwamba sababu ya upungufu wa wanafunzi wa kike  kitika vyuo vya ufundi ni jamii inayowazunguka watoto wetu,” anasema Dk Masika.
Anaeleza kwamba, watu wanaozunguka watoto hawa tangu awali, huwajenga mazingira ya kuamini kwamba, masomo ya sayansi ambayo ndiyo zao la wanafunzi wa ufundi, wanaume peke yao ndio wanaoweza kuyamudu.

“Ukipita kwenye shule nyingi za sekondari, utakuta wanafunzi wengi wa kike wanasoma masomo ya arts (sanaa), kwa hiyo mwisho wa siku hata wanaokuja kujiunga na vyuo vya ufundi wanakuwa wachache,” anasema Dk Masika.
Kutokana na hali hiyo,  Dk Mwasika anasema vyuo vya ufundi vya serikali vinajukumu kubwa la kuwavutia wanafunzi wa kike kusoma masomo ya ufundi.

Anasema katika kutekeleza jukumu hilo, Chuo cha Ufundi Arusha, kimejiwekea utaratibu wa kutembelea shule 20 za sekondari kila mwaka, lengo likiwa ni kuwashawishi wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na hatimaye kujiunga na vyuo vya ufundi.

“Tumeenda tena mbali zaidi, katika kila mahafali yetu huwa tunaalika shule moja ya wasichana ambapo huwa wanapata fursa ya kutembelea karakana zetu, kuelezwa mambo mbalimbali yahusuyo chuo ikiwa ni pamoja na kozi tunazofundisha,” anasema.

Kutokana na mikakati hiyo, anaeleza kuwa kwa sasa chuo hicho kinawanafunzi 672, ambao ni wastani wa ongezeko la asilimia 75 ya wanafunzi kutoka mwaka 2007.

Anaeleza kwamba, kati ya wanafunzi hao wasichana ni asilimia 18.
Anaongeza pia kwamba, chuo hicho kimeanzisha kozi nyingine mbalimbali ili kuwavutia vijana na haswa wasichana kujiunga na chuo hicho.

Kwa mujibu wa Dk Masika, moja ya kozi zilizoanzishwa  chuo hapo ni pamoja na ile ya  Uhandisi Umwagiliaji (Civil and Irrigation Engineering).

“Sababu nyingine ya kuanzisha kozi hii ni  kuunga mkono sera ya nchi ya Kilimo Kwanza, kwa sasa ni ATC pekee nchini inayotoa kozi hii,” anasema Dk Masika.
Anasema kabla ya kuanzisha kwa kozi hiyo, chuo hicho kilifanya utafiti na kubaini kuwa, pamoja na serikali kutaka kuwakwamua wananchi kupitia kilimo kwanza, kuna upungufu wa wahandisi wa kilimo cha umwagiliaji zaidi ya 8,200 nchini.

“Master Plan (Mpango kazi) ya kilimo cha umwagiliaji ya serikali, haiwezi kutekelezeka kwa mafanikio kama hakuna wataalam,” anasema.
Katika Mpango kazi wa Umwagiliaji wa Serikali (NIMP) wa mwaka 2002, Tanzania imetenga takribani hekta  29.4 milioni, kwa ajili ya utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji.

 Lakini,  mpaka kufikia Juni mwaka 2009, ni hekta 310,745  sawa na asilimia moja ndizo ambazo tayari zilikuwa zimeingizwa katika utekelezaji wa mpango huo.

Kwa mujibu wa maelezo yake Dk Masika, wataalam watakao zalishwa na ATC watasaidia sana kupunguza upungufu huo, huku akiwataka wasichana na wavulana kujiunga na fani hiyo ili kuweza kuziba pengo la mahitaji lililopo kwa sasa.

"Utafiti wetu ulibaini kuwa, watu wa sekta binafsi wanaogopa hata kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji licha ya kuwepo kwa frusa hiyo, tumebaini sababu inayowaogopesha ni pamoja na ukosefu wa wataalam wa kutosha katika nyanja hiyo,” anasema Dk Masika.

Anasema utafiti huo ulionyesha kwamba, sekta ya umma pekee ina upungufu wa wataalam hao 263 na kwamba wataalm wengene 1,659 watakuwa wanahitajika kwa kipindi cha muhongo mmoja ujao.

 Ingawa kilimo ni uti wa mgongo na kinategemewa na asilimia 80 ya Watanzania ambao wanahishi vijijini, takwimu zinaonyesha kwamba, mpaka sasa kinachangia asilimia 27 pekee katika pato la taifa la ndani (GDP).
Kuhusu uhai wa chuo, afisa  habari wake ,  Gaston Leseiyo, anasema  Chuo cha ufundi cha Arusha kilianzishwa mwaka 1978  kwa ufadhili wa Ujerumani kwa lengo la kusaidia sekta ya ufundi nchini.

Anaeleza kwamba, kwa muda wote huo kilikuwa kikitekeleza majukumu yake kikiwa chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, mpaka mwaka 2007 ambapo Taasisi ya Elimu ya Ufundi Nchini (NACTE), ilipokipa hadhi ya kujiendesha chenyewe.

 Anasema kwamba, chuo hicho kina wahadhiri 59 na kwamba kutokana na mikakati ya upanuzi wa chuo, kinalenga kuwa na jumla ya wahadhiri 100 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.Anaeleza kuwa, mbali na kuwa chuo cha ufundi pekee, ATC inajipanga kuwa kituo kikubwa cha Ufundi, Utafiti, Sayansi na Teknolojia kwa ukanda wa Afrika Mashariki mpaka kufikia mwaka 2025.

Comments

  1. l seeking the friends mobile +255766735297,+255718982444 lam obed mwisho from mbeya

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

Arusha Technical College strives for excellence